Mkali wa Afro Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’akiwapagawisha mashabiki wake.
Pamoja na watu kuwa wengi hadi wengine kurudishwa nyumbani, lile Tamasha la Wafalme limekamilika na shoo kabambe iliyotolewa na wafalme wawili, mkali wa Afro Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye kila mtu alikubali kwamba hakuna kama yeye Bongo na mfalme Mzee Yusuf.
Shoo hiyo ya kihistoria ilifanyika usiku wa kuamkia jana katika Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi kwenye Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.
Shoo iliyoshuhudiwa na mapaparazi wetu, ilianzia kwa waimbaji wa Kundi la Jahazi Modern Taarab ambao walitoa burudani za mwanzo huku wakiimba nyimbo mbalimbali zikiwemo zile zilizopo kwenye albam yao mpya inayojulikana kwa jina la Chozi la Mama.
Jahazi waliimba nyimbo nyingi kabla ya mfalme mwenyewe Mzee Yusuf hajapanda stejini.
Alipanda stejini saa 6:04 usiku ambapo kelele zilitawala huku mashabiki wakimwita babu..babu... babu... na kuanza rasmi kwa kupiga gitaa la besi kwa takribani dakika 16 na baadaye alihamia kwenye kinanda huku mkewe Leyla Rashid ‘Malkia’ akiimba na kuoneshana mahaba niue.